Jumapili 22 Novemba 2026 - 00:10
Haki ya kimataifa haipaswi kunyamaza mbele ya damu ya watoto wa Ghaza na Minab

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, katika ujumbe wake, amekosoa ukimya wa jumuiya ya kimataifa mbele ya mauaji ya watoto wa Palestina na Iran, huku akisisitiza umuhimu wa kusimamisha haki duniani.

Kwa mujibu wa taarifa ya kitengo cha tarajama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia nchini Pakistan, katika ujumbe wake wa kuadhimisha tarehe 20 Novemba, Siku ya Kimataifa ya Mtoto, amelaani kutojali jumuiya ya kimataifa mbele ya mauaji ya watoto wa Palestina na Iran. Aidha, ameitaja hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuhusu Waislamu wa Rohingya kuwa ni mwanga wa matumaini kwa mataifa yanayodhulumiwa.

Vilevile, amesisitiza kuwa Muqawama na msimamo thabiti wa Iran vimezifanya nguvu za dunia kutafakari upya madhara ya vita na matumizi ya silaha za nyuklia.

Ameongeza kuwa: “Siku hii inaadhimishwa katika maeneo mbalimbali duniani, wakati ambapo watoto wanaodhulumiwa wa Palestina na Iran bado wanasubiri kutimia kwa haki. Kutojali kwa jumuiya ya kimataifa mbele ya mauaji ya kimbari yanayofanyika Ghaza na mauaji ya watoto wasio na hatia kunatia wasiwasi mkubwa.”

Akizungumzia shambulio lililofanywa dhidi ya shule ya Minab, ameongeza kuwa: “Wakati wa shambulio hilo, watoto wadogo, wanawake na wazee walilengwa, licha ya kuwa wanafunzi walikuwa wakiendelea na masomo yao. Janga hili linatia mashaka madai ya wale wanaojinasibu kuwa watetezi wa amani na usalama duniani.”

Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia nchini Pakistan, akiendelea na ujumbe wake, amezungumzia hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuhusu Waislamu wa Rohingya, akisema: “Hukumu hii, iliyotolewa kufuatia kesi iliyowasilishwa na Gambia kwa kuungwa mkono na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), ni mwanga wa matumaini katikati ya giza la dhuluma na ukandamizaji. Inaweza kuwa ujumbe wa matumaini kwa mataifa yanayodhulumiwa duniani.”

Akizungumzia ukubwa wa janga la kibinadamu nchini Myanmar, amesema kuwa takribani Waislamu 10,000 wa Rohingya wameuawa, huku zaidi ya watu 700,000 wakilazimika kuacha nyumba na ardhi yao na kukimbia. Uhalifu huu umesababisha Pakistan na jumuiya ya kimataifa kutoa hisia za wasiwasi na kuitikia kwa namna mbalimbali.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi amesisitiza kuwa: “Kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya uhalifu uliofanyika Myanmar ni hatua muhimu. Hata hivyo, wananchi wanaodhulumiwa wa Ghaza nao bado wanasubiri haki ya kimataifa. Maelfu ya watu wameuawa katika eneo hilo, huku mamilioni wakilazimika kuyahama makazi yao na kubaki bila makazi wala msaada. Swali la msingi ni kwamba, ni lini wahusika wa uhalifu unaofanyika Ghaza watawajibishwa na haki itatendeka kwa wananchi wa Palestina?”

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, akizungumzia mkutano wa pande tatu uliofanyika Shenzhen, amesema: “Majuto na kurudi nyuma kwa madola yenye nguvu yanayotaka kuitawala dunia, pamoja na ujasiri na msimamo thabiti wa Iran, vimeyalazimisha madola hayo kutafakari tena masuala ya kimataifa, yakiwemo namna ya kuzuia matumizi ya silaha za nyuklia.”

Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Pakistan ameongeza kuwa: “Uchokozi dhidi ya Iran na matokeo yanayoweza kutokea kutokana na uchokozi huo vimezifanya nguvu za dunia kutambua ukweli kwamba matumizi ya silaha za nyuklia yanaweza kusababisha hali isiyoweza kudhibitiwa, kiasi kwamba huenda dunia isiweze tena kurejea katika hali yake ya kawaida. Kwa sababu hiyo, suala la kuzuia vita vya nyuklia na hata pendekezo la kuangamiza silaha hizo limeanza tena kupewa umuhimu.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, mwishoni mwa ujumbe wake, amebainisha kuwa: “Historia inathibitisha kwamba dhuluma na ukandamizaji hatimaye hushindwa mbele ya utashi na msimamo thabiti wa mataifa jasiri na huru.

Katika kumbukumbu za historia, mataifa na watu wanaobaki kuwa mifano ya kuigwa ni wale wanaohifadhi ujasiri, uthabiti na msimamo wao hata katika mazingira magumu zaidi.”

Amesisitiza kuwa kuunga mkono mataifa yanayodhulumiwa na kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha haki inapatikana katika medani ya kimataifa ni jambo la lazima lisiloweza kupuuzwa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha